Chuo Kikuu cha St John’s cha mkoani Dodoma kimefungwa baada ya wanafunzi
kususia mitihani wakituhumu na kupinga unyanyasaji wanaofanyiwa na
wahadhiri kwa kuwangusha kwenye mitihani na baadhi kuwabaka wanafunzi wa
kike.
Kwa mujibu wa Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Gabriel Mwaluko, wanafunzi
zaidi ya 290 wamesimamishwa masomo baada ya kukiuka sheria na kugomea
mitihani, hivyo chuo kimefungwa kikisubiri taratibu za kinidhamu
kuchukuliwa.
Awali uongozi wa serikali ya wanafunzi wa chuo ulieleza kuwa wanafunzi
290 wa St John’s na vyuo vikuu vishiriki vya Dar es Salaam
walisimamishwa masomo huku uongozi wa chuo ukiwapa barua za kuwaondoa
chuoni kuanzia wiki hii.
Habari hizo zilisema wanafunzi 196 wanaosoma Dodoma na wengine 94
wanaosoma katika vyuo vishiriki vya St. Mark's na Town Centre vya jijini
walipewa barua za kuondolewa chuoni.
Rais wa serikali ya wanafunzi, Andrew Chiduo, akizungumza na NIPASHE
Jumapili, alisema hatua ya kuwasimamisha inalenga kuwatisha ili
kuendelea kuwalinda walimu wanaodaiwa kuwanyanyasa na kuwadhalilisha na
kwamba wanasusia kufanya mitihani inayofanyika mwezi huu. Alisema
wahadhiri wanalazimisha kufanya ngono na wanafunzi wa kike, kuwabaka na
wale wanaokataa wanaangushwa kwenye mitihani.
Alisema katika tukio la hivi karibuni muhadhiri (jina tunalo)
alituhumiwa kumbaka mwanafunzi baada ya kumhadaa kumpa mitihani mingine
baada ya kushindwa ile aliyofanya mhula uliopita. Alisema wamelazimika
kugomea mitihani baada ya mhadhiri mmoja (jina linahifadhiwa)
kuwafelisha kwa makusudi wale wanaochukua kozi ya biashara wa mwaka wa
kwanza huku akiwapa vitisho.
Akijibu tuhuma hizo Profesa Mwaluko alisema madai ya mwalimu kumbaka
mwanafunzi yanachunguzwa kwa kuwahusisha polisi, kadhalika alisema
mhadhiri anayetuhumiwa kuwafelisha wanafunzi madai yake yanafuatiliwa
pia.
Chanzo: Gazeti la Nipashe
No comments :
Post a Comment