Dar es Salaam. Utumiaji wa dawa za kulevya umekuwa tatizo kubwa
linaloikumba dunia hasa wakati huu wa utandawazi, huku sehemu ya
waathirika wakuu wa dawa hizo wakiwa vijana ambao ni nguvukazi ya taifa.
Vijana wengi wanaotumia dawa za kulevya wamekuwa
wakieleza chanzo kikuu cha wao kujiingiza katika matumizi hayo ni
kushawishiwa na marafiki zao na ugumu wa maisha.
Hapa nchini vita ya dawa za kulevya imekuwa kubwa
kadri siku zinavyozidi kusonga mbele huku wahusika wakuu wakielezwa kuwa
ni vijana. Kundi hili ambalo ni nguvukazi ya taifa, wamekuwa
wakitumika kusafirisha sehemu mbalimbali za dunia na nyakati zingine wao
wenyewe wakitumia.
Mara kadhaa Serikali imekuwa ikitoa karipio kwa
wahusika kwa kutangaza vita dhidi ya waagizaji, wasafirishaji na
watumiaji ili kuhakikisha vita dhidi ya dawa za kulevya inatekelezwa kwa
vitendo jambo ambalo halijafanikiwa.
Katika uwanja wetu wa sauti za vijana, tuliwauliza, Vijana mnaishauri nini Serikali kuhusu vita dhidi ya dawa za kulevya? Hivi ndivyo walivyosema: Mshana Joseph(35): Tatizo lililopo hapa ni
wahusika wa dawa za kulevya ndiyo hao hao ambao wanatakiwa kusimamia na
kutekeleza sheria mbalimbali, hivyo ni jambo ambalo haliwezekani endapo
hakutakuwa na viongozi wenye uchungu na taifa lao kwani wataendelea
kuliangamiza taifa.
Mohamend Juma(25): Serikali inatakiwa kutambua
kuwa, waathirika wakuu ni sisi vijana hivyo itengeneze sheria kali kwa
wahusika ambao watakuwa wanabainika kujihusisha na vitendo vya uagizaji
na uuzaji, kwani bila kufanya hivyo ni dhahiri kwamba taifa litakosa
viongozi wa baadaye wengi watakuwa ni waathirika wa dawa hizo.
Alexander Timbati (39): Tuna kila sababu ya
kuilaumu Serikali kutokana na kufumbia macho watu ambao wamekuwa
wakijihusisha na usambazaji wa dawa hizo, Serikali inawajua ila
haiwachukulii hatua ni wakati sasa wa kufumbua macho na kuanza
kuwashughulikia kwa masilahi ya taifa.
Asteria Kanangi: Asante kwa mada nzuri, mimi
ninachokiona hapa ni kutokuwapo kwa usimamizi ipasavyo kwa sheria
zinazohusika, Serikali iwachukulie hatua kali wale wote ambao wanahusika
bila kujali cheo cha mtu na ikiwezekana wanyongwe kama China
wanavyofanya.
David Samson (27): Tuna kila sababu ya kuilaumu
Serikali kwa kushindwa kuwakamata wahusika, nimekuwa nikisikia bungeni
wabunge wakisema wanawajua wahusika, lakini baada ya hapo hakuna
chochote kinachoendelea, uzembe wa Serikali utakuja kuliweka njiapanda
taifa kwa kuoneana haya na kulindana.

No comments :
Post a Comment